WIZARA ya Maendeleo ya Jamii Jinsia na Watoto kwa kushirikiana na Mtandao wa Kutokomeza ukeketaji Tanzania, hivi karibuni iliendesha mkutano wa siku tatu katika ukumbi wa CCT mjini Dodoma uliokuwa na lengo la kujadili athari za mila hiyo hatari kwa wasichana na watoto wa kike.
Mila ambayo licha ya kupigwa vita na viongozi mbalimbali ikiwa ni pamoja vyombo vya habari na mashirika yasiyo ya kiserikali katika kila kona ya nchi ambayo jamii ya sehemu hizo inakumbatia mila hiyo, mila hiyo hatari inaonekana kuendelea kuwa sugu zaidi.
Mkutano huo ulihusisha wadau mbalimbali wanaopambana na mila hiyo yakiwemo mashirika mbalimbali yasiyo ya kiserikali yanayofanya shughuli zake za kupambana na mila hiyo katika mikoa ya Arusha, Kilimanjaro, Dodoma, Singida, Musoma, Iringa, Manyara,Tanga, Morogoro,Pwani, Dar es salaam na mikoa mingineyo ambako mila hiyo inafanyika zaidi ukilinganisha na mikoa mingine.
Baadhi ya mashirika yasiyo ya Kiserikali yanayopiga vita mila hiyo ni pamoja na AFNET Dodoma, WOWAP Dodoma, IAC matawi ya Dodoma, Kilimanjaro, Arusha, Tanga na Manyara, TAMWA, kituo cha sheria na haki za binadamu (LHRC), NAFGEM, AFNET Singida, TGNP, TAWLA, AYOHEP, IRA na mradi wa utafiti na utunzaji wa nyaraka wa chuo kikuu cha Dar es salaam (WRDP).
Ikumbukwe kuwa kwa mara ya kwanza Tanzania ilianza kushughulikia tatizo la ukeketaji mwaka 1994, baada ya mkutano wa kimataifa wa Cairo Misri, ambao ulipinga ukeketaji na kuhusisha na uvunjaji wa haki za binadamu, kwani suala la hilo lilionekana linaathiri zaidi maendeleo ya wasichana na wanawake na inapingana na haki za binadamu.
Pia katika mkutano wa wanawake uliofanyika Beijing China mwaka 1995 suala hili lilijitokeza na kuonekana kuwa ni tatizo ambalo linazidi kuwadidimiza wanawake kwa kunyimwa haki yao na kuwaathiri zaidi kisaikolojia.
Pamoja na kupigwa vita vitendo hivyo toka wakati huo, hali ya ukeketaji imekuwa bado ikiendelea katika jamii ya Watanzania hasa katika baadhi ya mikoa nchini, ambayo imeonekana kuikumbatia zaidi mila hiyo na kwa sasa kuanza kuifanya kwa siri kubwa.
Katika mkutano wa Afrika wa Mtandao wa Kutokomeza Ukeketaji uliofanyika Jinja Uganda March, 2000 uliazimia kila nchi mwanachama iwe na tawi la mtandao huo ili iwe rahisi katika utendaji kazi wa kila siku na kuleta mafanikio katika vita dhidi ya mila hiyo.
Hivyo Desemba, 2001 katika Hotel ya Njuweni Kibaha Mkoani Pwani tawi la mtandao wa kudhiti ukeketaji Tanzania lilizinduliwa likiwa na wajumbe 15, ikiwa ni sehemu ya mkakati wa serikali katika kupiga vita mila hiyo nchini na utekelezaji wa maazimio ya mkutano wa Afrika wa Mtandao wa kutokomeza mila hiyo.
Baada ya kuzinduliwa kwa tawi hilo nchini ambapo mwenyekiti wake ni Katibu Mkuu wa Wizara ya Maendeleo ya Jamii Jinsia na Watoto Bi. Hilda Gondwe, lilianza kufanya kazi yake kwa kutoa elimu na kuweka mikakati mbalimbali ya kuhakikisha kuwa mikoa inayoendeleza mila hiyo inaacha kufanya hivyo.
Mpaka sasa inaonesha kuwa Idadi ya mangariba waliosalimisha zana zao za kazi na kuacha ukeketaji katika mikoa ya Manyara (98), Dodoma (83), Singida (96) na kutoka katika mkoa wa Ruvuma ni Mangariba 202.
Katika mkutano huo wa mtandao wa kudhibti ukeketaji nchini ambapo mgeni rasmi alikuwa Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Bw.Musa Nkhangaa, akitoa hotuba yake ya ufunguzi aligusia suala muhimu sana katika vita ya kupambana na mila hiyo hatari.
Mkuu huyo alisema kama utawala bora utaimarika toka ngazi ya vitongoji, vita ya mila hiyo itakuwa na mafanikio makubwa kwani vitendo hivyo vinapofanyika jamii na viongozi wa sehemu husika hujua lakini huvifumbia macho.
Alisema kama viongozi katika ngazi za vitongoji na vijiji watakuwa na utawala bora basi kutakuwa na uhakika wa kushinda vita dhidi ya mila hiyo ambayo ni ukatili mkubwa kwa wanawake na watoto wanapofanyiwa vitendo hivyo.
Hapa napenda kumuunga mkono Mkuu wa Mkoa kwa kufichua ukweli juu ya tatizo hilo ambalo serikali na wafadhiri wamekuwa wakitumia fedha nyingi sana katika kupambana na mila hiyo, na bado inaendelea kufanyika.
Sikubaliani kuwa mtoto katika mtaa fulani atakeketwa halafu Balozi wa mtaa huo asifahamu kuwa kuna mtoto katika mtaa wake kafanyiwa kitendo hicho hatari ambacho huweza kumsababishia maumivu na hata kumuambukiza magonjwa mbalimbali ikiwemo UKIMWI.
Kuna kila sababu ya kuhakikisha kuwa viongozi hawa wanakuwa na elimu ya kutosha juu ya madhara ya mila hiyo ili wawe mabalozi wazuri katika kupiga vita ukeketaji ambao kwa sasa unafanyika kwa siri kubwa.
Kama kutakuwa na utawala bora kutoka ngazi hizo na viongozi hao wa mitaa wakagundua umuhimu wa kupiga vita mila hiyo hatari, Serikali pamoja mashirika yanayopiga vita, yatakuwa na kazi rahisi itakayofanikisha kumaliza kabisa tatizo hilo.
Kuhusu jambo hili serikali inatakiwa kuweka utaratibu maalum ambao utawabana viongozi wote wa mitaa na vijiji watakaoshindwa kutoa taarifa serikalini, ambao itabainika kuwa katika mitaa yao kuna watoto au wasichana wamefanyiwa ukeketaji.
Kwa kuwabana hivi ndio itakuwa rahisi kwao kutoa taarifa kwani kwa sasa inaonekana kama vile vita ya kupambana na mila hiyo inahusu viongozi wa serikali wa ngazi ya juu na si kutoka ngazi ya chini na mashirika fulani tu, hali inayosababisha jamii kuwa na mwitikio mdogo katika vita hiyo.
Katika utafiti wa mwaka 1996 uliofanywa na DHS ulibainisha kuwa ukeketaji umekithiri sana katika mikoa ya Arusha na Manyara 81%, Dodoma 68%, KIlimanjaro 37%, Iringa 27%, Singida 25%, Tanga 25%, Morogoro 20% na Dar es salaam 5.4% hali iliyoonesha kuwa kiwango cha ukeketaji nchini kipo juu sana kulingana na takwimu kutoka katika maeneo ya mikoa hiyo.
Hivyo kwa sasa baada ya serikali kuunga mkono vita dhidi ya ukeketaji, vitendo hivyo vimegeuka na kuanza kufanywa kwa siri zaidi hali inayosababisha madhara makubwa kwa waathirika wanaofanyiwa vitendo hivyo.
Imekuwa ni vigumu kwa mangariba wanaofanya vitendo hivyo kuwapeleka watoto na wasichana hao hospitali inapotokea matatizo, baada ya kuwafanyia vitendo hivyo kwa kuhofia kubanwa na sheria.
Hivyo hali imekuwa mbaya zaidi kuliko ilivyokuwa hapo awali ambapo wasichana waliokeketwa waliweza kupelekwa hospitali na kupata matibabu kama itatokea matatizo baada ya kufanyiwa kitendo hicho.
Vilevile kwa sasa watoto wadogo ndio hasa wanaofanyiwa vitendo hivyo ambao hawawezi hata kujieleza au kuhisi ni nini wanafanyiwa, hivyo kuwanyima haki yao msingi ya kutoa maamuzi kuhusiana na maumbile yao.
Kwa mfano hivi karibuni vyombo vya habari viliripoti habari kutoka Mkoani Singida ambapo mtoto mchanga alikeketwa, hali ambayo inasikitisha na kutisha kwa mtoto mdogo tena mchanga kufanyiwa kitendo hicho.
Hapa naungana na Mkuu wa Mkoa wa Dodoma kwa kuwatupia lawama viongozi wa ngazi ya vijiji na vitongoji kwa kutokuwajibika vilivyo kuzuia mila hiyo hatari ambayo inazidi kushika kasi katika baadhi ya mikoa hapa nchini.
Pia naiomba Serikali kuweka mikakati maalumu ambayo itahakikisha kuwa viongozi hawa wa ngazi za vijiji na vitongoji wanashiriki vilivyo katika kuhakikisha kuwa vitendo vya ukeketaji havitokei tena katika maeneo yao.
Kwa kufanya hivyo ikiwa ni pamoja na kutoa elimu kwa jamii juu ya madhara ya mila hiyo Serikali itakuwa imepiga hatua nzuri katika vita dhidi ya mila hiyo ambayo humnyima mwanamke haki yake.
Napenda kusisitiza kuwa kuendelea kwa mila ya ukeketaji nchini, viongozi wa ngazi ya vijiji na vitongoji wanawajibika kwa kuvifumbia macho vitendo hivyo huku wakielewa fika kuwa ni uvunjaji wa sheria na kinyume cha haki za binadamu kuendeleza mila hiyo.